SIKU YA WANAWAKE DUNIANI- MACHI 8
Machi 8 kila mwaka ni Siku ya Wanawake Dunia. Ili kuadhimisha siku hiyo kwa upande wa mpira wa miguu, TFF kwa kushirikiana na Chama cha Mpira wa Miguu cha Wanawake (TWFA) imeandaa mashindano mafupi kwa shule nane za sekondari za Mkoa wa Dar es Salaam.
Mashindano yataanza Februari 24 mwaka huu kwenye viwanja viwili vya Jitegemee Sekondari ambapo kutakuwa na kundi B wakati kundi A litacheza mechi zake Makongo Sekondari. Mechi zitaanza saa 8 mchana na kumalizika saa 10 jioni.
Kundi A lina shule za Makongo, Goba, Twiga na Lord Barden wakati Jitegemee, Benjamin Mkapa, Kibasila na Tiravi zitakuwa kundi B.
Lengo la mashindano ni kuhamasisha mpira wa miguu kwa wasichana katika ngazi ya shule, kuandaa, kubaini na kuendeleza mafanikio yanayopatikana katika timu ya wanawake ya Taifa.
Pia kutoa fursa kwa watoto wa kike kusherehekea Siku ya Wanawake duniani kupitia mpira wa miguu, kutekeleza ushiriki wa TFF katika shughuli za kijamii na ni sehemu ya mchakato wa kuandaa mashindano ya ligi kwa wasichana.
Uchaguzi wa timu shiriki umezingatia mchango wa shule katika kuendeleza mpira wa miguu kwa wasichana/wanawake. Pia zawadi zitatolewa kwa mshindi wa kwanza, pili na tatu.
Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya Mashindano hayo ni Zainab Mbiro kutoka Twiga Sekondari wakati wajumbe ni Brighton Mbasha (Jitegemee), Yusuf Mohamed (Tiravi), Michael Bundala (TFF), Furaha Francis (TFF/TWFA) na Rose Kissiwa (TWFA).
Tunaomba wadau mbalimbali wajitokeze kusaidia gharama za uendeshaji wa mashindano hayo.
FAINALI FDL KUANZA MACHI 17
Hatua ya fainali ya Ligi Daraja la Kwanza (FDL) itafanyika kuanzia Machi 17 mwaka huu katika kituo ambacho kitatangazwa baadaye.
Timu tatu kutoka katika kila kundi ndizo zitakazocheza fainali hiyo. Washindi watatu wa juu ndiyo watakaofuzu kucheza Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) msimu ujao.
Mikoa mitatu ya Mbeya, Mwanza na Ruvuma imewasilisha maombi ya kuwa wenyeji wa fainali hizo. Maombi hayo yanafanyiwa uchambuzi kabla ya kutangaza mkoa uliopewa nafasi hiyo.
Wakati huo huo, michuano ya Ligi Daraja la Kwanza (FDL) hatua ya makundi inamalizika kesho (Februari 22 mwaka huu) kwa mechi tatu za kundi A.
Polisi Dar es Salaam watakuwa wenyeji wa Morani FC ya mkoani Manyara katika mechi itakayochezwa Uwanja wa Mabatini ulioko Mlandizi mkoani Pwani.
Mgambo Shooting Stars ya Tanga itaoneshana kazi na Temeke United ya Dar es Salaam katika mchezo utakaofanyika Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga wakati Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro utashuhudia mechi kati ya wenyeji Burkina Faso na Transit Camp ya Dar es Salaam.
Boniface Wambura
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)
No comments:
Post a Comment