TAARIFA KWA UMMA.
UTANGULIZI
Baadhi ya Magazeti ya tarehe 17 Februari 2012 yaliandika habari zisizo sahihi kuhusiana na kikao cha Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) cha tarehe 16 Februari 2012 kilichohusu hesabu za Wizara ya Maliasili na Utalii za mwaka 2009/10.
Magazeti hayo yaliliripoti kuwa baadhi ya fedha zilizokusanywa katika kipindi hicho hazikupelekwa Hazina, kila gazeti likinukuu kiasi chake cha fedha, na mengine yakataja kuwa kulikuwa na ufisadi kuhusiana na suala hilo.
Habari hiyo ihusuyo ufisadi siyo ya kweli kwa kuwa fedha zote zinazotakiwa kupelekwa Hazina kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii hupelekwa Hazina, isipokuwa zile za mifuko maalum ambayo ilianzishwa kisheria, kama vile Mfuko wa Kuhifadhi Wanyamapori Tanzania (Tanzania Wildlife Protection Fund – TWPF) ambao ndiyo uliohojiwa siku hiyo.
Ufafanuzi ulitolwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii Bibi Maimuna Tarishi mbele ya Kikao hicho cha PAC na muafaka ukafikiwa kuwa Wizara itakaa tena na Wakaguzi ili kufafanua zaidi kuhusu Mfuko wa TWPF na sheria inayotawala taratibu zake za utendaji.
MFUKO WA TWPF NI KWA MUJIBU WA SHERIA
Mfuko wa Kuhifadhi Wanyamapori Tanzania (TWPF) ni mfuko wa Serikali ulianzishwa kwa Sheria ya Bunge Namba 21 ya mwaka 1978. Aidha, Sheria ya Uhifadhi wa Wanyamapori Namba 5 ya mwaka 2009 iliendelea kutambua mfuko huo katika Kifungu cha 91 (1) cha Sheria hiyo.
Vyanzo vya fedha zinazoingia kwenye Mfuko wa TWPF vimeainishwa katika Kifungu cha 91 (3) cha Sheria ya Uhifadhi wa Wanyamapori Namba 5 ya mwaka 2009 kuwa ni:
(i) asilimia 25 ya maduhuli yatokanayo na Wanyamapori,
(ii) mauzo ya vitu vilivyotaifishwa chini ya Sheria ya Uhifadhi wa Wanyamapori,
(iii) fedha zitokanazo na utalii wa picha nje ya Hifadhi za Taifa na Ngorongoro.
Kazi zinazogharimiwa na mfuko wa TWPF zimeainishwa katika Kifungu cha 9 (2) cha Sheria ya Uhifadhi wa Wanyamapori Namba 5 ya mwaka 2009, baadhi yake zikiwa kama ifuatavyo:
(i) kuzuia ujangili;
(ii) kulinda wananchi na mali zao kutokana na wanyama wakali na waharibifu;
(iii) kugharimia miradi inayowanufaisha wananchi wanaoishi katika vijiji vinavyopakana na mapori;
(iv)kufanya utafiti wa wanyamapori;
(v) kuelimisha kuhusu uhifadhi wa wanyamapori kwa kutumia Klabu za Malihai;
(vi) kuwafunza askari wa wanyamapori.
Mfuko hugharimia shughuli hizo baada ya mipango yake kupitishwa na Bodi ya Utendaji ya Mfuko wa TWPF.
Mfuko wa TWPF hukaguiwa na Wakaguzi wa Serikali kutoka Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG). Kwa mwaka 2009/10 Hoja ilihusu kwa nini fedha za mfuko huo zisipelekwe Hazina kwanza ndipo zirudishwe kwenye mfuko.
Hoja hiyo ilitolewa maelezo tarehe 16 Februari 2012 na Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii Bibi Maimuna Tarishi ambaye alitoa ufafanuzi mbele ya Kamati ya PAC kuwa Mfuko huo ulianzishwa na Sheria, hivyo taratibu za kukusanya mapato, pamoja na utendaji wake, hutawaliwa na Sheria husika.
Mwenyekiti wa PAC Mheshimiwa John Cheyo alihitimisha mjadala huo kwa kuagiza kuwa wakaguzi wakae tena na Wizara ili kupata maelezo zaidi kuhusu Mfuko wa TWPF na sheria inayotawala taratibu zake za utendaji.
IDADI YA WATALII INAJULIKANA
Suala jingine lililoripotiwa isivyo na baadhi ya magazeti ya tarehe 17 Februari2012 ni kuwa Wizara haina takwimu za watalii walioingia nchini mwaka 2009/2010.
Habari hiyo siyo kweli kwa kuwa idadi ya watalii wanaoingia nchini kila mwaka inajulikana. Kwa mfano, kwa mwaka 2009 watalii waliotembelea Tanzania ni 714,367 ambao walilingizia taifa mapato ya Sh. Milioni 1,511,704.59 (takriban Trilioni 1.5). Aidha, kwa mwaka 2010 idadi ya watalii ilikuwa 782,699 ambao waliingiza Sh. Milioni 1,767,967.85 (takriban Trilioni 1.7).
Katika kikao cha PAC cha tarehe 16 Februari 2012 Hoja ilihusu ni kwa nini takwimu zote za Wizara hazikutunzwa sehemu moja. Katibu Mkuu aliitolea hoja hii ufafanuzi kuwa takwimu zipo ila kila Idara inatunza takwimu zake. Aliongeza kuwa kwa sasa mifumo inaboreshwa ili takwimu zote ziweze kuwekwa pamoja chini ya Mkurugenzi wa Sera na Mipango.
HITIMISHO
Wizara ya Maliasili na Utalii itaendelea kufanya kazi pamoja na Wakaguzi kutoka Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ili kutekeleza maagizo yote yaliyotolewa na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali.
[MWISHO]
George Matiko
MSEMAJI WA WIZARA
WIZARA YA MALIASILI NA UTALII
20 Februari 2012
No comments:
Post a Comment