Friday, February 17, 2012

MKUU WA MKOA AIPONGEZA HALMASHAURI YA SINGIDA KWA KUBORESHA SEKTA YA AFYA IKIWEMO KUJENGA VITUO VYA AFYA.

Mkuu wa mkoa wa Singida Dk.Kone akisalimiana na baadhi ya viongozi wa kijiji cha Mpambaa.
Jengo jipya la zahanati ya kijiji cha Mpambaa.(Picha na Nathaniel Limu).
Na Nathaniel Limu.
Mkuu wa mkoa wa Singida Dkt. Parseko Vicent  Kone ameipongeza halmashauri ya wilaya ya Singida, kwa juhudi zake za kuboresha sekta ya afya ikiwemo kujenga  majengo mapya ya vituo vya afya na zahanati yaliyo na ubora wa hali ya juu.
Amedai kuwa majengo hayo yanafanana kabisa na thamani ya fedha zilizotumika.
Dkt. Kone amesema hayo wakati akizungumza kwenye mkutano wa hadhara uliyofanyika katika kijiji cha Mpambaa tarafa ya Mtinko wilaya ya Singida, muda mfupi baada ya kuweka jiwe la msingi la zahanati ya kijiji hicho.
Mkuu huyo wa Mkoa Dkt. Kone amesema amejifunza au ameona  hata kazi ya ukarabati wa vituo vya afya na zahanati mbalimbali katika halmashauri hiyo ni wa kiwango cha juu mno na unafanana na thamani halisi ya fedha zilizotumika.
Katika hatua nyingine, Dkt. Kone amewapongeza wakazi wa kijiji hicho kwa kuwa mstari wa mbele kuchangia kwa hali na mali jenzi wa zahanati hiyo mpya.
Mkuu huyo wa mkoa amesema katika taarifa za ujenzi wa zahanati hizo tatu, wananchi wa vijiji hivyo wamechangia nguvu kazi na fedha taslimu sio chini ya shilingi milioni 14.”Hongereni sana”,na kuongeza; kwa kuwaambia kuwa “Endeleeni kuchangia miradi yenu ya maendeleo bila kuchoka, kwa njia hiyo mtakuwa mnaivutia serikali na wadau mbali mbali, kuharakisha kuwaunga  mkono katika kukamilisha miradi yenu.  Lakini kama mkidanganyika na  kuacha kuchangia miradi yenu, kwa hakika kitendo hicho kitachangia kudumaza maendeleo yenu”.
Wakati huo huo, mkuu huyo wa mkoa,amewataka kuanzia sasa kuelekeza nguvu zao katika jenga nyumba za kuishi watumsihi wa zahanati hizo ili kuharakisha  kuanzishwa  kwa huduma ya afya.


Kikundi cha uhamasishaji cha kijiji cha Mpambaa kikitoa burudani kwenye mkutano wa hadhara ulioitishwa kwa ajili ya mkuu wa mkoa wa Singida Dk.Kone akizungumza na wananchi.
Mkuu wa mkoa wa Singida Dk.Parseko Vicent Kone akizungumza na wananchi wa kijiji cha Mpambaa tarafa ya Mntinko wilaya Singida muda mfupi baada ya kuweka jiwe la msingi la zahanati ya kijiji hicho.
Mkuu wa wilaya ya Singida Pascal Kulwa Mabiti akisalimia wananchi wa kijiji cha Mpambaa muda mfupi kabla ya kumkaribisha mkuu wa mkoa Dk.Kone kuzungumza na wananchi hao.

No comments:

Post a Comment