Jaji Mwanahamisi Kwariko.
Nathanel Limu.
Mahakama kuu kanda ya Dodoma inayoendelea na vikao vyake mjini Singida imemwamuru mshitakiwa Simon Andrew mkazi wa kijiji cha Kidaru wilayani Iramba, kupelekwa kwenye taasisi inayojishughulisha na magonjwa ya akili kwa kipindi chote cha maisha yake yaliyobakia hapa duniani.
Akitoa amri hiyo, Jaji Mwanahamisi Kwariko amesema mahakama yake imekubaliana na upande wa mashitaka kwamba mshitakiwa Simon alimuua bibi kizee Tiale Mbogo kwa kukusudia.
Aidha, Jaji Kwariko amesema mahakama pia inakubaliana na upande wa mashitaka kwamba wakati mshitakiwa Simon akitenda kosa hilo hakuwa na akili timamu.
“Mahakama hii imepokea ripoti kutoka kwa daktari kuwa mshitakiwa ni mgonjwa sugu wa afya ya akili, Kwa hali hiyo, mahakama imefiakia uamuzi kuwa mshitakiwa Simon apelekwe kwenye taasisi inayojishughulikia watu wenye magonjwa ya akili”,amesema.
Awali mwanasheria mkuu wa serikali Neema Mwanda, alidai mbele ya Jaji Kwariko kuwa mnamo Desemba 18 mwaka 2000 katika muda usiofahamika, mshitakiwa alimuuwa kwa makusudi kikongwe Tiale Mbogo.
Neema amesema kuwa mshitakiwa Simon alikutwa na majirani wa bibi kikongwe Tiale akiwa amesimama jirani na mwili wa Tiale.
Watu hao waliweza kumkamata mshitakiwa na kumfikisha mbele ya vyombo vya dola.
Imedaiwa bibi Tiale kabla ya kufikwa na mauti hayo, alikuwa akiota jua. Mshitakiwa alimpiga na kitu ambacho hakijafahamika na kisha kufariki dunia papo hapo.
Wakati huo huo, Kesi ya kupinga matokeo ya ushindi wa ubunge wa mbunge wa jimbo la Singida mashariki Tundu Lissu inatarajiwa kuanza kuungurma wakati wo wote kuanzia sasa..
Akizungumza na mwandishi MO BLOG ofisini kwake,kaimu hakimu wa mahakama ya hakimu mkazi mkoa wa Singida Flora Ndale amesema maandalizi ya kikao hicho yanaendelea vizuri.
“Ni kweli kuwa kesi hiyo ipo. Kwa sasa sijafahamishwa tarehe rasmi ya kuanza kusikilizwa kwa kesi hiyo ya kupinga matokeo yaliyompa Tundu Lissu ubunge. Lakini itaanza wakati wo wote kuanzia sasa”, alisema na kuongeza kuwa “nakuomba tuendelee kuwasiliana ili nitakapojua tarehe rasmi ya kusikilizwa kwa kesi hiy ,niweze kukufahamisha kwa manufaa ya jamii”.
Kesi hiyo ambayo imeanza kuvuta hisia kwa wakazi wa mkoa huu, inatarajiwa kufanyika kwenye jengo jipya la mahakama ya mwanzo Utemini jirani na shule ya msingi ya Utemini manispaa ya Singida.
CHANZO MO-BLOG
No comments:
Post a Comment