POULSEN ATAJA 23 KUIVAA MSUMBIJI
Kocha wa timu ya Taifa (Taifa Stars), Jan Poulsen leo (Februari 16 mwaka huu) ametangaza kikosi cha wachezaji 23 kwa ajili ya mechi ya mchujo ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) ambalo fainali zake zitafanyika mwakani nchini Afrika Kusini.
Kabla ya kuivaa Msumbiji kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam katika mechi itakayochezwa Februari 29 mwaka huu, kikosi hicho kinatarajia kucheza mechi ya kirafiki Februari 23 mwaka huu dhidi ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC) itakayofanyika kwenye uwanja huo huo.
Wachezaji wapya walioitwa kwa mara ya kwanza kwenye kikosi hicho kitakachoingia kambini Februari 20 mwaka huu jijini Dar es Salaam ni viungo Jonas Gerald (Simba) na Salum Abubakar (Azam).
Kikosi kamili kinaundwa na makipa Shabani Kado (Yanga), Juma Kaseja (Simba) na Mwadini Ali (Azam). Mabeki ni nahodha Shadrack Nsajigwa (Yanga), Masoud Cholo (Simba), Aggrey Morris (Azam), Juma Nyoso (Simba), Juma Jabu (Simba), Stephen Mwasika (Yanga) na Kelvin Yondani (Simba).
Viungo ni Jonas Gerard (Simba), Shabani Nditi (Mtibwa Sugar), Shomari Kapombe (Simba), Salum Abubakar (Azam), Mwinyi Kazimoto (Simba) na Abdi Kassim (Azam).
Washambuliaji ni Hussein Javu (Mtibwa Sugar), John Bocco (Azam), Nizar Khalfan (Philadelphia Union, Marekani), Mrisho Ngasa (Azam), Ally Badru Ally (Canal Suez, Misri), Uhuru Selemani (Simba) na Nsa Job (Villa Squad).
AFC NAYO YASHUKA DARAJA
Timu ya AFC ya Arusha imeshindwa kutokea kwenye mechi ya Kundi C ya Ligi Daraja la Kwanza (FDL) dhidi ya 94 KJ iliyokuwa ichezwe jana (Februari 15 mwaka huu) kwenye Uwanja wa Mabatini ulioko Mlandizi mkoani Pwani.
Kwa mujibu wa Kanuni ya 21 ya FDL timu yoyote inayoshindwa kufika kituoni na kusababisha mchezo husika kutochezwa itashushwa daraja hadi Ligi ya Taifa na matokeo ya michezo yake yote itafutwa ili kutoa uwiano sahihi kwa timu zilizobaki kwenye mashindano.
Si Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), msimamizi wa ligi hiyo Kituo cha Pwani wala Kamishna wa mechi hiyo Ramadhan Mahano waliokuwa na taarifa yoyote ya mapema juu ya AFC kushindwa kufika kituoni.
AFC ambayo mbali ya kushushwa daraja inatakiwa kulipa faini ya sh. milioni moja kabla ya kucheza Ligi ya Taifa msimu ujao. Sh. 500,000 kati ya hizo zitakwenda kwa timu ya 94 KJ iliyoingia gharama za kujiandaa kwa mechi hiyo ambapo wapinzani wao hawakufika uwanjani.
Kundi C la ligi hiyo sasa linabakiwa na timu nne baada ya Manyoni FC ya Singida nayo kushuka daraja kwa kushindwa kucheza mechi yake dhidi ya Polisi Tabora iliyokuwa ifanyike Februari 12 mwaka huu Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi mjini Tabora.
Timu zilizobaki katika kundi hilo ambalo baada ya mbili kujitoa hakuna itakayoshuka daraja ni 94 KJ ya Dar es Salaam, Polisi Tabora, Polisi Morogoro na Rhino FC ya Tabora.
Boniface Wambura
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).
No comments:
Post a Comment