Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amemteua Bibi Amina Saidi Mrisho kuwa Kamishna wa Sensa ya Mwaka 2012.
Aidha, Rais Kikwete amemteua Bibi Seraphia R. Mgembe kuwa Mratibu wa Mpango wa Kurasimisha Raslimali na Biashara za Wanyonge Tanzania (MKURABITA).
Taarifa iliyotolewa na kutiwa saini Dar es Salaam leo, Jumanne, Februari 21, 2012, na Kaimu Katibu Kiongozi, Bwana Peniel Lyimo imesema kuwa uteuzi huo umeanza jana, Februari 20, mwaka huu, 2012.
Taarifa ya Bwana Lyimo imesema kuwa kabla ya uteuzi wake, Bibi Amina Mrisho alikuwa Mkuu wa Mkoa wa Pwani.
Katika taarifa tofauti iliyotolewa na kutiwa saini pia mjini Dar es Salaam leo, Jumanne, Februari 21, 2012, na Katibu Mkuu Ikulu, Bwana Peter Ilomo, imesema kuwa uteuzi huo wa Bibi Mgembe umeanza pia jana, Jumatatu, Februari 20, 2012.
Bwana Ilomo amesema katika taarifa yake kuwa kabla ya uteuzi wake Bibi Mgembe alikuwa Mkurugenzi wa Utawala na Fedha wa MKURABITA.
Bibi Mgembe anachukua nafasi iliyoachwa wazi na Bwana Ladislaus Salema ambaye amestaafu kwa mujibu wa sheria.
Mwisho.
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu.
Dar es Salaam.
21 Februari, 2012
No comments:
Post a Comment