Rais Mstaafu wa awamu ya tatu, Benjamin Mkapa.
Rais Mstaafu wa awamu ya pili, Ali Hassan Mwinyi.
Makamu Mwenyekiti wa CCM (Bara) Mstaafu, John Malecela.
-Ni mabadiliko makubwa katiba ya CCM
-Viongozi wastaafu kuwa na baraza lao
HALMASHAURI Kuu ya Taifa (NEC) ya Chama cha Mapinduzi (CCM), imewaondoa rasmi viongozi wa taifa wastaafu kwenye vikao vya Kamati Kuu (CC) na Nec na badala yake wameundiwa baraza la ushauri.
Viongozi walioondolewa ni Rais Mstaafu wa awamu ya pili, Ali Hassan Mwinyi; Rais Mstaafu wa awamu ya tatu, Benjamin Mkapa; Makamu Mwenyekiti wa CCM (Bara) Mstaafu, John Malecela; Rais Mstaafu Zanzibar wa awamu ya tano Zanzibar, Dk.
Salmin Amour na Rais Mstaafu wa Zanzibar wa awamu ya sita, Abeid Aman Karume.
Aidha, wajumbe wa Nec watakaochaguliwa kupitia wilaya watakuwa ni viongozi wa kazi za muda wote ili kuweka wazi zaidi wajibu wa wajumbe hao kuwa karibu na wanachama wa kushughulikia shida zao.
Kwa maana hiyo, makada watakaochaguliwa kuingia NEC kupitia wilayani hawatakuwa wabunge wala wawakilishi.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini Dodoma jana, Katibu wa NEC wa Itikadi na Uenezi wa chama hicho, Nape Nnauye, alisema waliondolewa kuwa wajumbe wa Nec ni marais wastaafu wa Jamhuri ya Muungano ambao walikuwa wenyeviti wa CCM Taifa.
Alisema wajumbe wengine walioondolewa katika ujumbe wa NEC ni marais wastaafu wa Zanzibar ambao pia walikuwa ni makamu wenyeviti wa CCM Zanzibar na makamu wenyeviti wa CCM Bara.
“Baraza litakuwa na kazi ya kutoa ushauri kwa Chama cha Mapinduzi na serikali zinaoongozwa na CCM kwa madhumuni hayo katika jambo mahsusi,” alisema Nape.
Alisema wajumbe wa baraza hilo wanaweza pia kualikwa ama wote au mwakilishi wao kuhudhuria vikao vya Chama ngazi ya Taifa.
Alisema katika marekebisho hayo ya Katiba ya CCM ya mwaka 1977 toleo la mwaka 2010 na kanuni zake, NEC imeongeza idadi ya wajumbe kutoka 200 hadi 300.
Pia alisema kuwa idadi hiyo ya wajumbe wa Nec imeongezeka kutokana na makundi mapya ya wajumbe yaliyobainishwa kwenye katiba hiyo.
Aliyataja makundi hayo kuwa ni wajumbe wa Nec ngazi ya taifa ambao ni 20 kati yao 10 kutoka Tanzania Bara na 10 Tanzania Visiwani na wajumbe 10 wa kuteuliwa na Mwenyekiti wa chama hicho.
Makundi mengine ni wajumbe wanaoingia kwa nafasi zao ambao ni Mwenyekiti, Waziri Mkuu, Spika wa Bunge, Makamu wa Rais, Rais wa Zanzibar na Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar.
Pia aliyataja makundi mengine kuwa ni wajumbe wanaotoka kwenye vyombo vya uwakilishi ambao ni wabunge 10 na wawakilishi watano kutoka Baraza la Wawakilishi Zanzibar.
Nape alisema kundi lingine ni la wajumbe 221 wanaochaguliwa kutoka wilayani na watakaochaguliwa katika nafasi hizo ni wale viongozi wa kazi za muda wote kama vile wenyeviti wa wilaya, ili kuweka wazi zaidi wajibu wa wajumbe hao kuwa karibu na wanachama na kushughulikia shida zao.
“Hii yote bado ni utekelezaji wa dhana ya kujivua gamba, tulisema dhana hii itagusa maeneo mengi na eneo hili ni la kuhakikisha chama kinasogea karibu na wanachama,” alisema Nnauye.
Alisema kupitia nafasi hizo za wilaya wanachama wa chama hicho watawakilishwa vizuri ingawa katika ngazi ya mikoa, bado Mwenyekiti na Katibu wa chama hicho wa mkoa wanabaki kuwa wajumbe wa Nec.
Nape alisema kundi lingine la mwisho kuwa ni la wajumbe wanaochaguliwa kutoka kwenye Jumuiya za chama ambao ni Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) nafasi 15 ambapo Tanzania Bara ni nafasi tisa na Zanzibar sita. UVCCM ni nafasi 10 Tanzania bara sita na Zanzibar wanne wakati Jumuiya ya Wazazi watano ni kutoka Bara ni watatu na Zanzibar wawili.
Katika tukio lingine, mwanasiasa mkongwe wa CCM, Kingunge Ngombale-Mwiru, ameibua hisia za wajumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM, baada ya kukataa utaratibu wa kuwapata wajumbe wa kikao hicho katika ngazi ya wilaya.
Kwa mujibu wa chanzo kutoka ndani ya kikao hicho, Ngombale-Mwiru alitaka wajumbe hao wapatikane kutoka mkoa badala ya wilayani kama ililivyokuwa katika Katiba ya sasa ya chama.
Hata hivyo, kabla ya Nape kuzungumza na waandishi wa habari kutangaza maamuzi hayo, alikanusha taarifa kuwa wabunge hawataruhusiwa kugombea nafasi ya ujumbe wa NEC kupitia CCM ngazi ya wilaya.
Alizungumza na NIPASHE kwa simu, alisema kumekuwa na taarifa zinazotolewa na vyombo vya habari kwamba wabunge wamepigwa marufuku kugombea ujumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM kupitia wilaya wanazotoka wakati ukweli hakuna agenda kama hiyo ndani ya chama hicho.
“Mimi ndiyo msemaji wa chama, kwa hiyo nisikilize mimi siyo vyombo vya habari, nasema hakuna ajenda ya kuwazuia wabunge kugombea NEC wilaya kama inavyoelezwa,” alisema Nape ambaye hata hivyo hakufafanua zaidi suala hilo.
Taarifa kwamba wabunge wamepigwa marufuku kugombea NEC wilaya pia zilibainishwa na wabunge wenyewe juzi wakati Rais Jakaya Kikwete, alipokutana nao katika kikao kilichofanyika ukumbi wa White House mjini Dodoma juzi.
Katika kikao hicho vyanzo vya habari vinasema Mbunge wa Sikonge, Said Nkumba, ndiye aliyegusia suala la wabunge wa CCM kuzuiwa kugombea nafasi za ujumbe wa NEC kupitia wilayani na kumuomba Rais Kikwete awape ufafanuzi kuhusiana na suala hilo.
Kutokana na madai hayo ya wabunge, Rais Kikwete ambaye ni Mwenyekiti wa CCM Taifa, alijibu kuwa hakuna mpango wa kuwazuia wabunge kugombea nafasi za NEC katika mabadiliko ya katiba ya chama hicho.
Kwa muda mrefu mambo ambayo yamekuwa yakipingwa na wabunge wa CCM kuhusiana na marekebisho ya katiba ni lile linalotaka wabunge wasigombee nafasi yoyote ya ujumbe wa NEC.
Pendekezo hilo likipitishwa, wabunge wanaotaka kuwania uras watakuwa na nafasi ndogo ya kupitishwa kwani hawatakuwa wajumbe wa NEC wa wilaya.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment