Wednesday, February 22, 2012

HOSPITALI YA ST.CAROLUS SINGIDA KUTUMIA ZAIDI YA SHILINGI MILIONI 250 KUGHARAMIA NYUMBA ZA WATUMISHI.

Mkuu wa mkoa wa Singida Dkt .Parseko Kon akisalimiana na wafanyakazi wa hospitali ya St.Carolus iliyopo kijiji cha Mtinko wilayani Singida.
Lango kuu la kuingilia hospitali ya St. Carolus  ya kijiji cha Mtinko wilayani Singida. (Picha zote na Nathaniel Limu).
Na.Nathaniel Limu
Hospitali ya St.Carolus iliyopo katika kijiji cha Mtinko wilayani Singida inatarajia kutumia zaidi ya shilingi milioni 252.8 kugharamia ujenzi wa nyumba za kuishi watumishi wake.
Akitoa taarifa yake kwa mkuu wa mkoa wa Singida Dk.Parseko Kone muda mfupi kabla ya kuweka jiwe la msingi kwenye majengo hayo yanayoendelea kujengwa Mganga Mawidhi wa hospitali hiyo Dkt. Peter Mtaro amesema fedha hizo ni msaada kutoka shirika la masista wa Upendo wa Mt. Karoli Borromeo la nchini Ujerumani na Uholanzi.
Dkt. Mtaro amesema wamefikia uamuzi wa kujenga nyumba hizo ili kuhakikisha kuwa kila mtumishi anakuwa na nyumba yake ya kuishi katika mazingira ya kumwezesha kutoa huduma kwa urahisi zaidi.
Aidha, amesema hospitali hiyo ina wafanyakazi 123 na kati ya hao asilimia 70 wana nyumba za kuishi na asilimia 30 wanaishi maeneo yaliyo nje ya hospitali.
Amesema ujenzi wa nyumba hizo unaendelea vizuri na kwamba mkandarasi ameahidi kumaliza ujenzi huo mei mwaka huu.
Wakati huo huo, Mkuu wa mkoa wa Singida Dkt. Kone ameahidi kuwa atafanya juhudi kuhakikisha hospitali hiyo inapata msaada wa vitanda vya wagonjwa ili kupunguza uhaba wa vitanda uliopo.

Mkuu wa mkoa wa Singida Dkt. Parseko Kone (wa pili kushoto) akikagua majengo ya nyumba za wafanyakazi wa hospitali ya St.Carolus ya kijiji cha Mtinko wilaya ya Singida. Kushoto ni mganga mfawidhi wa hospitali hiyo Dkt. Peter Mtaro.

No comments:

Post a Comment