Mussa Juma, Arumeru.
CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimetangaza ratiba yake ya kushiriki uchaguzi mdogo wa Jimbo la Arumeru Mashariki, Arusha huku wanachama wake wanne wakiwa tayari wamejitokeza kuomba kuteuliwa.
"Chama cha Chadema kinawahakikishia … kitashiriki katika uchaguzi huo mdogo wa Arumeru Mashariki, kwa lengo la kushinda,” alisema Mkurugenzi wa Habari na Uenezi wa Chadema, John Mnyika katika taarifa yake jana.
Alisema fomu zilianza kutolewa tangu jana na kwamba mwisho wa kuchukua na kurejesha fomu ni Februari 25.
Mnyika alisema fomu zinatolewa katika Ofisi ya Chadema ya Wilaya ya Arumeru, Maji ya Chai-USA River na pia katika Ofisi za Chadema za Mkoa wa Arusha.
“Baada ya hapo vikao vya chama vinavyohusika na uteuzi vitafanyika ili kumpata mgombea mmoja,” alisema.
Uchaguzi huo unafanyika baada ya kifo cha aliyekuwa Mbunge wa jimbo hilo hilo, Jeremia Sumari.
Mnyika alisema anaamini umakini na uimara ambao kimeendelea kuudhihirisha katika kuwatumikia na kuwawakilisha Watanzania, kitashinda.
Mchakato wa uteuzi ngazi ya jimbo na wilaya utafanyika kati ya Februari 26 na 29, mwaka huu wakati uteuzi ngazi ya taifa utafanyika Machi 3 Machi mpaka 4.
Waliochukua fomu
Wanachama wa Chadema waliojitokeza kutaka kupeperusha bendera ya chama hicho ni Joshua Nasari, Samweli Shami, Francis Tembo na Mwenyekiti wa Baraza la Wanawake Wilaya ya Arumeru (Bawacha), Anna Mwagirwa.
Kujitokeza kwa wanachama hao wanne wa Chadema, kunafanya idadi ya waliojitokeza kuwania kiti hicho kufikia sita. Juzi, wanachama wawili wa CCM walichukua fomu kupitia chama hicho.
Waliojitokeza ni pamoja na mtoto wa Sumari, , Sioi na Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa CCM Taifa, William Ndeoya Sarakikya.
Mwenyekiti wa Baraza la Vijana la Chadema Mkoa wa Arusha, Ephata Nanyaro alisema wanachama hao wanatarajiwa kuanza kupewa fomu za kugombea leo.
Alisema utaratibu wa kura kumpata mgombea wa chama hicho, unatarajiwa kutangazwa mara baada ya kukamilisha kikao cha sekretarieti ya Chadema, Dar es Salaam.
Sarakikya akana
Katika hatua nyingine, William Sarakikya aliyechukua fomu juzi kugombea ubunge wa jimbo hilo kupitia CCM, amesema kwamba si mtoto wa Mkuu wa Majeshi Mstaafu Jenerali, Mirisho Sarakikya.
Akizungumza jana mjini Arusha, Sarakikya alisema kwamba wote ni wa ukoo mmoja lakini hajazaliwa na Mkuu huyo wa majeshi wa zamani.
Wakati William akikanusha, Jenerali Sarakikya naye alisema jana kwamba mgombea huyo anatokea katika ukoo wake, lakini siyo mtoto wake wa kumzaa.
“Kimsingi ukoo wote wa Sarakikya ni ndugu lakini William siyo mtoto wangu wa kumzaa, ni mtoto wa jamaa yangu. Mimi nina watoto wanne ambao hawako kabisa kwenye siasa,” alisema Mstaafu huyo wa jeshi na kutaja kazi za wanaye hao kuwa ni udaktari, uhandisi ualimu na taaluma ya benki.
Chanzo mwananchi.
No comments:
Post a Comment